Wanawake wajasiliamali zaidi ya sabini mjini Tunduma wilayani Momba mkoa wa Songwe wamefundishwa namna ya kurasimisha biashara zao ili waweze kuzitumia fursa za kibiashara zilizoko mipakani mwa nchi kwa lengo la kuepukana na changamoto wanazokumbana katika biashara hizo.
Mafunzo hayo yalitolewa jana na kampuni ya Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) inayolenga kuwaendeleza kibiashara wanawake wajasiliamali hapa nchini.
Taassisi zilizoalikwa kuwaelimisha wajasiliamali hao kuhusiana na taratibu mbalimbali za kibiashara ni pamoja na Uhamiaji Tunduma, TRA, Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Momba , Idara ya Biashara Halmasauli ya Momba , SIDO Mkoa wa Mbeya TCCIA, SACCOS, VICOBA, TFDA na TBS
Wakinamama hao walifundishwa jinsi ya kupata mitaji, kukuza na kuendeleza biashara zao kwani wanawake wengi wanaofanya biashara hizo wanashindwa kunufaika na fursa zilizopo nje na ndani ya nchi kutokana na kuwa na mitaji midogo na kukosa elimu ya ujasiliamali.
Mmoja wa wawezeshaji katika mafunzo hayo Leons Mtana alitoa sababu ya kuwaelimisha wajasiliamali hao kuwa ni kufanya biashara zao ziweze kutambulika kwa mamlaka husika ikiwemo kuwa na leseni ya biashara,kuwa na tini namba na kulipa mapato halali.
Mtana aliongeza sababu nyingine kuwa kusajili majina ya kampuni kunasaidia biashara zao kuweza kuthibitishwa na Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) kwa lengo la kutangaza biashara zao na kuzifanya zikubalike katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo Rehema Ulivia ambaye ni mwenyekiti katika jukwaaa la wanawake kitengo cha miradi Mji wa Tunduma amewaasa wakinamama wa Tunduma kujitokeza kwa wingi zinapotokea fursa kama hizo
‘’Nimejifunza faida ya kufanya biashara nje ya nchi, na nimeelewa nifuate taratibu gani kuweza kufanya biashara na nchi jirani na nawashauri wakinamama wakisikia fursa kama hizi wajitokeze kwa wingi ’’ alisema Rehema
Kwaupande wake Pili njebele ambaye ni mjasiliamali mjini hapo alisema kuwa kutokana na mafunzo hayo, amejifunza jinsi ya kuendesha biashara zake ndogondogo na kuziendeleza ziwekubwa ili aweze kupata mtaji wakumuwezesha kufanya biashara za kuvuka mpaka.
Licha ya hayo, Majuma Hamza ambaye ni Afisa mtendaji wa Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) amewashauri kina mama wasifanye biashara kinyemela bali watumie njia halali kwasababu wakikamatwa wanalipishwa pesa nyingi ambayo ingesaidia katika kuongeza mtaji katika biashara zao.
Hata hivyo, Tunduma ni mji uliopo kwenye mpaka wa Tanzania na Zambia ambapo pia ni lango la kuingilia na kutokea katika nchi jirani kama Zambia na Jamuhuri ya Kidemokrasia Ya Congo, mji huo unasifika kwa biashara unazidi kukua kutokana na mzunguko wa watu ikiwa ni pamoja na wageni kutoka nchi jirani na wenyeji.
No comments:
Post a Comment